Ninafuraha kuungana na nyinyi leo
kwa hiki kitendo ambacho kitaandikwa kwa kumbukumbu kama maandamano makubwa ya
ukombozi katika salua ya taifa letu.
Miongo kumi iliyopita mwamerikani
shujaa ambaye nyuma ya kivuli cha mnara wake tumesimama leo, aliweka saini kwa
hati ya azimio ya mapinduzi. Hiyo amri ilikuja kama mhimili angavu ya matumaini
kwa mamilioni ya watumwa wenye ngozi nyeusi ambao walikuwa wakiteketezwa kwa
hari ya dhuluma kali. Ilikuja kama alfajiri ya shangwe baada ya kifungo cha
usiku mrefu.
Lakini miaka mia moja baadaye, mtu
mweusi bado hana uhuru. Miaka mia moja baadaye, maisha ya mtu mweusi bado
imelemezwa kwa pingu za ubaguzi na nyororo za unyanyapaa.
Miaka mia moja baadaye, mweusi
anaishi katika kiziwa pweke cha umaskini akizingirwa na bahari ya ukwasi wa
mali na maendeleo
Miaka mia moja baadaye, mweusi
anaendelea kuzorota akiwa pembeni mwa jamii ya Marekani na anajipata akiwa
mkimbizi nchini mwake mwenyewe. Hiyo basi tumekuja hapa leo kuigiza hali hii ya
aibu.
Kwa njia moja tumekuja hapa kwenye
kitivo cha taifa letu kutaka kukidhiwa cheki. Waanzilishi wa jamhuri yetu
waliandika mambo ajibu katika katiba na tangazo la uhuru, walitilia saini cheti
cha muamana ambacho kila Mmarekani alistahili kuwa mrithi.
Hii hati ilikuwa agano kuwa watu
wote, ndiyo watu weusi pamoja na watu weupe walihakikishiwa haki yao halisi ya
uhai, huria na kutafaraji.
Ni bayana leo kwamba Marekani imeasi
hiyo hundi kwa kutazama maisha ya wananchi wake walio na rangi ngozini. Badala ya
kutii huu mkataba adhimu, Marekani imempa mtu mweusi hundi bandia, hundi ambayo
imerudishwa imeandikwa “hakuna pesa” lakini tumekataa kuamini kwamba benki ya
haki imetiwa taflisi. Tumekataa kuamini kuwa kuna ufukara kwenye hazina ya
uadilifu ya taifa hili. Kwa hivyo tumekuja kuwasilisha hii cheki- cheki ambayo
kwa kuwasilishwa itakidhi utajiri wa uhuru na uhifadhi wa haki. Pia tumekuja
mahali hapa stahifu kukumbusha Marekani ajila moto moto ya wakati huu. Sasa sio
wakati wa kutabaradi na kujikokota kwa maringo ama kumeza dawa za kutuliza
maumivu ili tiba iahirishwe hadi badaye.
Sasa ni wakati wa kudai ahadi zote za kidemokrasia. Sasa ndio wakati wa
kuamka kutoka kwa giza na bonde hafifu la kutengwa na kuingia kwa baraste
angavu ya uhaki kwa wote. Sasa ndio wakati wa kuinua taifa letu kutoka kwa
mchangarau mwepesi wa uonevu na kuipeleka kwa mwamba thabiti wa kiundugu. Sasa
ndio wakati wa kufanya haki kuwa dhahiri kwa watoto wote wa Mungu.
Itakuwa hali ya kuponza kama taifa
litapuuzilia hii hima ya wakati huu. Huu msimu wa masika ya kutoridhika kwa
mweusi hautapita hadi tuwe na msisimko wa kiangazi cha uhuru na usawa. Elfu
moja mia kenda na sitini na tatu sio mwisho ila ni mwanzo. Wale walio na
matarajio kuwa mweusi alihitaji tu kupwita na kutoa stima mwilini kisha
atatosheka watapata pigo la mshtuko mkali kama taifa litarudi kuwa
hali-kawaida. Hakutakuwa na kumpumzika wala tabaradi Marekani hadi mweusi apate
haki yake ya raia huru. Kimbunga kali cha kukaidi kitaendelea kutetemsha
misingi ya taifa letu hadi siku yenye mwangaza wa haki utapoingia.
Lakini kuna jambo lazima niwaambie
watu wangu ambao wamesimama kwa ukingo vuguvugu unaoelekea kwenye kasri ya
uadilifu. Katika harakati ya kupigania mahala petu stahiki, tusipatikane na
hatia ya kutenda uhalifu. Heri tusikate kiu ya utashi wa uhuru kwa kukunywa
kutoka kombe la hasira na chuki.
Milele lazima tufanye mapambano yetu
tukiwa kwa daraja ya juu kuzingatia uanadamu na nidhamu. Tusiruhusu ubunifu wa
vita hivi uporomoshwe kuwa wa mabavu. Tena na tena, lazima tuinuke kwa madaha
na kujibu vita vya mabavu kwa vita vya kiroho. Mbinu hii mwafaka ya vita ambayo
imekumbatiwa na jamii ya mweusi inafaa itutoe kwa kuwashuku wazungu wote kwa
ujumla kwa kuwa wengi wa ndugu zetu weupe, jinsi wamedhihirisha kwa kujitokeza
kwao hapa leo, wameshakubali kuwa mustakabali wao umeshikana na wetu.
Wameshakubali kuwa uhuru wao umeambatana barabara na uhuru wetu. Hatuwezi
kutembea pekee yetu.
Tunavyotembea, lazima tuahidi kuwa
tutaendelea kusonga mbele. Hatuwezi kurudi nyuma. Kuna wale wanaowauliza
watetezi kabambe wa haki za uraia, “Mtatosheka lini?” hatuwezi kutosheka kamwe
kama mweusi ndiye mpokezi wa dhuluma za kuhofisha za ukatili wa polisi. Hatuwezitosheka
kama bado miili zetu, wakati zimechoka kutokana na usafiri mrefu haziwezipata
mapumziko kwenye mikahawa barabarani wala kwenye hoteli za jijini.
Hatuwezikutosheka kama bado maendeleo ya mtu mweusi ni tu kutoka kijiji duni
kidogo na kuhamia kijiji duni kikubwa. Hakuna vile tutatosheka kama bado watoto
wetu wanavuliwa utu wao na kuibiwa uungwana wao na mabango milangoni
yalizoandikwa “Watu weupe pekee” hatuwezi kutosheka kama mweusi mzawa wa
Mississippi hawezi kupiga kura na mweusi kutoka New York anaamini hata hana
haja ya kupiga kura hiyo. La, la hatujatosheka na hatutatosheka hadi haki
itiririke chini kama maji na wema kama mto mkubwa.
Na si kuwa sinafahamu kwamba wengine
wenyu mmefika hapa kutokana na majaribio na mateso mengi. Wengine wenu wamekuja
hapa kutoka rumande hivi majuzi. Wengi kutoka sehemu ambazo malilio yenyu ya
kutafuta haki iliwaacha na mapigo ya mawimbi ya kusulubiwa na kufuatwa na upepo
wa ukatili wa polisi. Mmekuwa mashujaa kwa kuteseka kwa kiubunifu. Endeleeni
kufanya kazi kwa imani kuwa mateso na kudhulumiwa huvutia ukombozi.
Rudini kule Mississippi, rudini kule
Alabama, rudini kule Carolina Kusini,
rudini kule Georgia, rudini
kule, Louisiana, rudini kule vijijini
duni na kwa majiji yetu ya Kaskazini mkijua hii hali inawezabadilishwa na
itabadilishwa. Tusiendelee kufadhaika kwenye bonde la kutamauka.
Nawambieni leo, marafiki zangu,
ingawa tunakabiliwa na shida hizi leo na kesho, bado niko na ndoto. Ndoto iliyo
na mizizi thabiti kwenye ndoto ya Marekani.
Ninayo ndoto kuwa siku moja nchi hii
itainuka na kutekeleza mambo halisi ya huu mwito: “Tunaamini ukweli huu kuwa
dhahiri: kuwa wanadamu wote waliumbwa wawe sawa.”
Ninayo ndoto kuwa siku moja kwenye
milima nyekundu ya Georgia wana wa watumwa wa kale na wana wa mabwenyenye wa
kale wataketi pamoja kwa meza moja ya undungu.
Ninayo ndoto kuwa siku moja hata
jimbo la Mississippi, jimbo linaloteketea kwa joto la dhalala na kuteketea kwa
joto la minyanyaso, litabadilika liwe kisima cha huru na haki.
Ninayo ndoto kuwa wanangu wane ambao
ni wadogo siku moja wataishi kwa taifa ambalo hawatathaminiwa kwa rangi ya
ngozi yao ila kwa uwezo na kitiba yao.
Ninayo ndoto leo
Ninayo ndoto kuwa siku moja, kule
Alabama na wabaguzi wake sugu, na gavana wao mwenye midomo yenye kudondoka maneno
kejeli na yenye kukebehi, siku moja huko huko Alabama watoto wachanga wanaume
na wasichana weusi watashikana mikono na watoto wachanga wavulana na wasichana
weupe kama ndugu na dada.
Ninayo ndoto leo
Ninayo ndoto kuwa siku moja kila
bonde litainuliwa, na kila kilima na mlima utashushwa, mahali penye matuta
patalainishwa na penye gurufa patanyooshwa na utukufu wa Mungu utatokelezea na
watu wote watauona kwa pamoja.
Hii ndio matumaini yetu. Hii ndiyo
imani nitarudi kusini nayo. Kwa hii imani tutawezakuchomoa kijiwe cha kukomboa
kutoka mlima mkubwa wa kubana. Kwa hii imani tutaweza kugeuza makelele udhia ya
taifa letu kuwa wimbo mahili wa undungu. Kwa hii imani tutawezafanya kazi kwa
pamoja, kusali pamoja kuteseka pamoja, kufungwa gerezani pamoja, kupigania haki
zetu pamoja, tukijua kuwa siku moja tutakuwa huru.
Hiyo ndio itakuwa siku, hiyo ndio
itakuwa siku ambayo watoto wote wa Mungu wataimba kwa kuipa maana mpya, “Nchi
yangu, ni nchi yenye utamu wa huru, na hivyo ninaimba. Nchi ambayo babu zangu
waliishi, nchi ya sifa ya kuwa ya kuhijiwa kutoka pande zote za milimani acha
kengele ya huru zilie.”
Na kama Marekani itakuwa taifa
kubwa, haya lazima yafanyike. Kwa hivyo acha kengele ya huru zilie kutoka juu
ya vilima potevu vya New Hampshire. Acha kengele za huru zilie kutoka kwa
milima kubwa ya New York. Acha kengele za huru zilie kutoka milima yenye urefu
usio na kifani wa Pennsylvania!
Acha kengele za huru zilie kutoka
vilele vyenye kofia za theluji za Rockies Colorado!
Acha kengele za huru zilie kutoka
magema yaliyokunjika ya California!
Lakini sio hayo tu; acha kengele za
huru zilie kutoka mlima wa mwamba wa Georgia!
Acha kengele za huru zilie kutoka
mlima unaotazama wa Tennessee!
Acha kengele za huru zilie kutoka
kila kilima na kichuguu cha Mississippi. Kutoka pande zote za mlima, acha
kengele za huru zilie.
Na
hayo yatakapofanyika, tutaporuhusu
kengele za huru zilie, zitapolia kutoka kila kijiji na kila boma, kutoka
kila jimbo na kila jiji, tutawezakuharikisha ile siku ambayo kila mtoto wa Mungu,
weusi na weupe, Wayahudi na watu wa mataifa, Waprotestani na Wakatoliki
watawezakushikana mikono na kuimba wimbo wenye maneno ya kidini ya mtu mweusi “
Niko huru mwishowe! Niko huru mwishowe! Ahsante Mola wema, tuko huru mwishowe!”
Its good and well understood able
ReplyDelete.
Thank you
Delete